Posted by Mjengwa | Tuesday, October 04, 2011
MEATU nasi tumo aliye tabasamu nyuma ya aliyevaa shati jekundu
(Updated 6:29PM) MATOKEO UCHAGUZI IGUNGA
Baada ya kufuatilia matokeo kwa muda mzima wa jana mitandao ya FikraPevu na JamiiForums inaamini kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka mshindi wa kinyang’anyiro cha Ubunge jimbo la Igunga baada ya kupata kura zaidi ya 26,000 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kimepata kura zinazokaribia 23,000. Ukijumlisha na kura zote ambazo zimepigwa CCM imeshinda kwa karibu asilimia 49 huku CDM kikiwa na asilimia 45. Hata jumla ya matokeo mengine yote yangeenda kwa CDM bado CDM isingeweza kushinda.
Ushindi huo wa CCM umehitimisha mojawapo ya michuano mikali ya kisiasa nchini ambapo vyama vya CDM, CUF na CCM vilionekana kufukuzana vikali. Mshindi wa kiti hicho cha Ubunge
ni Dr. Peter Dalaly Kafumu ambaye kabla ya nafasi yake hiyo alikuwa ni Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini. Mshindani wake mkuu huko Igunga alikuwa ni Mwalimu Kashindye wa CDM.
Licha ya matatizo ya hapa na pale upigaji kura ulifanyika katika hali ya amani na utulivu mkubwa. Kiasi cha wapiga kura hata hivyo kilienda sambamba na kile cha waliopiga kura katika uchaguzi uliopita na hivyo kuonesha kuwa pamoja na kampeni motomoto za huko Igunga bado haikupatikana njia ya kuwashawishi watu wengi zaidi kujitokeza kupiga kura.
Ushindi wa CCM umekuja na kuwa pigo kubwa kwa CDM na hivyo kukifanya chama hicho kushindwa kushinda uchaguzi mdogo hata katika mazingira ambayo kilitarajiwa au kuonekana kukubalika zaidi. Chaguzi nyingine ambazo CDM ilidhaniwa kushinda ni ile ya Babati, Busanda na Biharamulo ambako kote CCM iliweza vyema kuvitetea viti vyake.
Uchaguzi huu umefanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa Igunga Bw. Rostam Aziz kujiuzulu nafasi zake ndani ya chama – ikiwemo Ubunge – na hivyo kusababisha kuitishwa uchaguzi mdogo miezi michache baada ya kushinda.
Hata hivyo kitakwimu, CDM imetoa ushindani mkali dhidi ya CCM
kama ilivyotarajiwa. Katika uchaguzi uliopita CCM ilishindwa kwa zaidi ya asilimia 70 huku ikipata kura zaidi ya 35,674 huku CUF ikipata kura 11,321. CDM haikuwa na mgombea. Ni wazi kuwa kitakwimu tu CCM imepunguza kura zake lakini ni punguzo ambalo limetosha bado kukipatia ushindi na kazi kubwa ilikuwa kwa CDM kuweza kukabili idadi hiyo kubwa.
Matokeo hayo yamepokewa kwa mshangao mkubwa na baadhi ya viongozi wa CDM ambao wameonekana kushangazwa na mwelekeo huo hasa baada ya matokeo ya Igunga Mjini kuonekana kuwa hayakuw akama yalivyotarajiwa mahali ambapo ilionekana ni ngao
yao. “Kwa kweli hatujui nini kimetokea, lakini kuna mengi ya kujifunza” amesema mmoja wa viongozi hao wa kitaifa aliyezungumza nasi bila kutajwa jina
lake kwani matokeo yalikuwa hayajatolewa rasmi.
Jedwali la matokeo ya awali kwa kadiri tulivyoweza kuyapata yanaonesha matokeo kuwa hivi.*
KATA | CCM | CDM |
|
Ntobo | 730 | 302 |
|
Nguvumoja | 694 | 284 |
|
Nkinga | 1484 | 1079 |
|
Itumbo | 1079 | 590 |
|
Nango | 897 | 645 |
|
Igurubi | 1064 | 801 |
|
Mwisi | 926 | 992 |
|
Mbutu | 1335 | 1427 |
|
Kinungu | 855 | 756 |
|
Bukoko | 1136 | 931 |
|
Nyandekwa | 691 | 613 |
|
Ndembezi | 866 | 806 |
|
Chabutwa | 545 | 581 |
|
Ziba | 1053 | 860 |
|
Igoweko | 1051 | 808 |
|
Mwamashija | 806 | 590 |
|
Sungwizi | 1225 | 718 |
|
Isakamaliwa | 525 | 593 |
|
Ngulu | 622 | 412 |
|
Choma | 1227 | 918 |
|
Kininginila | 700 | 451 |
|
Mwashiku | 798 | 484 |
|
Simbo | 738 | 1016 |
|
Itunduru | 738 | 784 |
|
Mwamashinda | 1224 | 1421 |
|
Igunga | 3181 | 3358 |
|
JUMLA | 26190 | 22220 |
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Naye Katibu Mwenezi wa Itikadi wa NEC ya CCM Bw. Nape Nnauye ametangaza kupitia mtandao wa JamiiForums.com kuwa chama chake kimeibuka mshindi. Akitupa vijembe vya kisiasa Bw. Nape amesema kuwa “MAGWANDWA NOMAAAAA kelele zote hizo aibu hii sasa inakuaje? kati ya kata 22 mmeambulia 3 CCM ikiibuka na 18 cuf moja tu, masikini”
* Matokeo hayo si rasmi bali kwa kadiri ya vyanzo vyetu mbalimbali yanawakilisha kwa kiasi kikubwa idadi kamili na hayatotofautiana
sana na matokeo yatakayotangazwa rasmi. Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa wakati wowote na Msimamizi wa Uchaguzi huo Mdogo jimbo la Igunga.
Hizi ndizo sababu za ushindi wa CCM Igunga
Friday, 09 September 2011 12:28 newsroom
UNA mambo ambayo watu wengine hawataki kusikia kabisa. Wenye mwono na tafakuri za hisia, wataibuka na kusema CCM itabwagwa vibaya Igunga. Nilianza kujifunza aina hizo za watu wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana, ambapo rafiki yangu aliwahi kunieleza kwamba rais angekuwa Dk. Willibrod Slaa. Nilimpinga kwa nguvu zote, maana alijivisha miwani ya chuma. Nilicheka sana, tena nikamweleza, pamoja na usomi wake na ujuzi wake wa kuchambua na kuchanganua mambo, upeo wake umekomea kutanguliza hisia badala ya uhalisia.
Ilikuwa inatakiwa uwe mwendawazimu kusema rais angeshinda Dk. Slaa, maana haikuhitaji uchambuzi na utafiti unaokutanisha jopo la maprofesa kudhihirisha hilo, kwani hata mtoto tu angeweza kujua kwamba, Dk. Slaa hakuwa na ubavu wa kushinda urais bali kuwa mshindani.
Kwangu mimi Dk. Slaa alikuwa mshindani na si mshiriki. Hilo lilikuwa wazi na hata yeye alijua kwamba hatashinda urais, bali ataleta ushindani kisiasa. Kwa kweli unaweza kuonekana mwehu, mwendawazimu na juha kwa kueleza ukweli, lakini wenye kuona mbali watakuunga mkono. Kwa nini nasema hivyo?
Mpaka sasa wapo wanaodhani kwamba vyama vya upinzani vikiongozwa na CHADEMA na CUF, vitaweza kushinda dhidi ya CCM Igunga.
Siwashangai, maana uchambuzi wa hisia unatawala na kuacha ukweli ambao wanauficha kwa makusudi.
SABABU ZA CCM KUSHINDA
Kama ambavyo ameeleza Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kwamba ushindi wa CCM Igunga hauna shaka, kutokana na uhalisia wa historia za CCM jimboni humo, ndivyo nami navyomaanisha hapa.
Nape anasema kuna sababu nyingi za ushindi lakini kuna sababu kuu tano, ambazo zitakifanya Chama kuibuka na ushindi.
Mosi, Chama kilichokuwa kinashikilia jimbo hilo kabla kujiuzulu kwa mbunge wake Rostam Azaz, ni Chama Cha Mapinduzi. Hivyo kulingana na wingi wa kura kilichopata, bado kinakuwa na kiashiria kizuri cha kushinda tena.
Lakini pamoja na kwamba kilikuwa kinashikilia jimbo hilo, kinakwenda kushindana na vyama vingine vinane vya upinzani, jambo ambalo ni dhahiri CCM, ina uwezo mkubwa wa kuibuka mshindi kwa kuwa upinzani watagawana kura.
Ni ukweli kwamba CUF na CHADEMA vimekuwa na wapenzi wengi, kwa hali hiyo tu, dawa yao dhidi ya CCM ilikuwa kuungana. Lakini kwa kila kimoja kusimamisha mgombea inatoa fursa kwa CCM kupita katikati yao.
Pili, hakuna shaka kwamba katika kura za maoni za kumpata mgombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu, alipata kura 588. Kwa kutazama hilo tu, ni wazi hizo ni hesabu nzuri za ushindi.
Kwani mgombea wa CHADEMA alipata kura 63 kati ya wapiga kura za maoni 369. Hilo halina shaka kwamba, CHADEMA wana kazi zaidi ya kumuuza mgombea wao.
Maana kwa mtu anayekubalika kupata kura hizo na kushindwa kupata hata robo ya kura zote, ni dalili ya wazi kwamba hakubaliki.
Tatu, Nape anasema Igunga kulikuwa na tatizo la bei ya pamba, na Mkuu wa Mkoa wa Tabora alikwenda kuagiza wafanyabiashara wapandishe bei na wakafanya hivyo.
Lakini katika harakati hizo, CHADEMA wao wakafanya juhudi za kutaka kupinga kupanda kwa bei hiyo, wakati wakijua ina manufaa kwa wananchi katika kuinua kipato chao.
Kama wananchi wataamsha hasira zao juu ya CHADEMA, basi ni wazi chama hicho kitaangukia pua katika uchaguzi huo, jambo ambalo linatarajiwa kutokea.
Nne, mara nyingi ushindi wa vyama vya upinzani hutegemea mpasuko na makundi yanayoibuka wakati wa kura za maoni za kumpata mgombea wa CCM. Wakati huu hilo halipo.
Wagombea wote walioshiriki katika kura za maoni za CCM wameridhika na kilichotokea na kumpa ushirikiano mkubwa mgombea mwenzao. Turufu nyingine ya ushindi.
Kwa kuwa hakuna mpasuko na kwa kuwa wagombea waliona taratibu zilizingatiwa na aliyepatikana ni chaguo la wengi, umoja wa CCM Igunga umeshawamaliza wapinzani.
Tano, madiwani wa Jimbo la Igunga wapo 35 na CCM ina madiwani 32. Madiwani watatu tu wanatoka upinzani. Kwa hesabu hizo tu, mwenye kujua maana na hesabu za kisiasa, anaweza kujua nani mwenye uwezo wa kushinda ubunge Igunga.
Haina maana kwamba kwa kuwa CCM ina madiwani wengi basi hata mgombea anakubalika. Unaweza kuwa na madiwani wengi lakini mbunge akawa hakubaliki.
Kinachoipa ushindi CCM sio wingi wa madiwani pekee, bali sababu kuu tano kwa ujumla wake, ambazo zinaonyesha ni kwa namna gani, CCM itaibuka na ushindi Igunga.
Kwa jumla, kuna mambo mengi ya kujivunia katika Jimbo la Igunga, mambo yaliyofanywa na Rostam Aziz.
Huwezi kusahau kutaja elimu, afya, maji na miundombinu. Kwa jumla, CCM watakuwa wako kifua mbele kwa mafanikio hayo.
Kwa kuwa upinzani wamekuwa na sera za kuzusha na kupaka watu matope, maendeleo ya sekta muhimu za kijamii na kiuchumi zitakuwa zinawafunga mdomo.
Mambo hayo yanaibeba kwa kushirikiana na sababu zile tano za kisayansi katika kukifanya Chama Tawala, kuendelea kushikilia kiti hicho.
Lakini kwa kuwa mfumo wa vyama vya siasa vililetwa ili vyama vingine vishiriki na vingine vishindane na hatimaye kupata kimoja cha ushindi, haina budi kuona upinzani ukijaa Igunga.
Kuchukua ushindi wa mezani sio mzuri, kama kushiriki katika ushindani, maana vyama vitatu vya CHADEMA, CUF na CCM vinashindana, lakini kwa kuwa CHADEMA na CUF vimeshindwa kujua mbinu za ushindi, wameiacha CCM ikiwapiga chenga.
Kuna kupigwa chenga za kiutu uzima, lakini chenga watakazopigwa Igunga zitakuwa za kitoto kwa maana wameshindwa kujua namna watakavyobwagwa.
Ni heri wangejua kitakachowafika Oktoba 2, maana hakuna shaka watakimbia kabla hata ya matokeo kutangazwa. Ningefurahi kama Mbowe, Lipumba na Dk. Slaa wangesubiri matokeo Igunga.
Tathmini ya Ushindi wa CCM
Friday, 09 September 2011 12:26 newsroom
MASIKIO, pengine na macho ya wadau wa siasa walioko ndani na nje ya Tanzania, kwa kipindi hiki yataelekezwa jimbo la Igunga mkoani Tabora. Hali hiyo inatokana na kiu ya wengi kutaka kujua mwenendo na hatima ya kisiasa ya jimbo hilo katika mchakato unaoendelea, wa kumpata mbunge mwingine wa jimbo hilo. Uchaguzi mdogo wa kumpata mbunge mpya, unafanyika baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Rostam Aziz, kuachia ngazi Julai mwaka huu, kutokana na sababu ambazo wafuatiliaji wengi wa masuala ya siasa za Tanzania bila shaka wanazijua. Kipenga cha kufanyika uchaguzi mdogo katika jimbo hilo kwa mara ya kwanza kilipigwa pale Spika wa Bunge, Anna Makinda, alipotanga kujiuzulu wa Rostam, na kufuatiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kulitangaza jimbo hilo kuwa wazi.
Vyama vya siasa vyenye nia ya kulitwaa jimbo hilo lililokuwa chini ya Chama Cha Mapinduzi, vimeshaingia jimboni kupigana vikumbo.
Vyama vilivyoingia kwenye kinyang'anyiro hicho ni CCM ambayo imemsimamisha Dk. Dalaly Kafumu, CUF (Leopard Mahona), CHADEMA (Joseph Kashine), CHAUSTA (Hassan Lutengama), UPDP (Hemed Ramadhani), AFP (Steven Nushuyi), DP (Saidi Cheni), SAU (John Maguma), na UMD iliyemteua Lazaro Ndegea, ambaye amejitoa katika dakika za mwisho.
Wakati kampeni zilianza rasmi Agosti 7, 2011, vyama hivyo vimepiga kambi jimboni humo kwa ajili ya kuweka misingi imara itakayoviwezesha kuwaweka sawa wapigakura ambao ndiyo mtaji wa kila chama kuibuka na ushindi.
Ukiachilia mbali sera na uhodari wa chama kupiga kampeni, vipo vigezo vingine ambavyo vinaweza kuwa viashiria vya awali kwa chama kuweza kupata ushindi katika uchaguzi huo.
Miongoni mwa viashiria hivyo ni kutokana na jinsi chama husika kilivyojijenga jimboni, kilivyoimarika, na idadi ya wanachama kilio nao ukiondoa mashabiki na wapenzi wa kawaida watakaopiga kura.
CCM sera zake zinaeleweka vyema kuliko vyama vingine vyote inavyoshiriki navyo katika uchaguzi huo. Kadhalika inao wanachama wengi na hata wapenzi na mashabiki wa kawaida, kutokana na ukweli kwamba hata wanachama na mashabiki walio wengi wa vyama vya upinzani, ni walewale ambao wamekuwa upande wa CCM.
Matarajio ya CCM
Tangu kipenga kilipopulizwa, CCM imekuwa ikisema kwa kujiamini kwamba itashinda uchaguzi huo, ikianisha vigezo ambavyo itavitumia kikamilifu kufikia ushindi.
Akizungumzia mikakati ya Chama Cha Mapinduzi, Mratibu wa Kampeni za CCM jimboni humo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba, anathibitisha ushindi wa Chama chake kwa kuainisha vigezo maalum.
CCM ikilinganishwa na vyama vingine, ndicho chenye madiwani wengi ambao ni 32 katika jimbo hilo, na CHADEMA inafuata lakini kwa mbali, ikiwa madiwani watatu tu katika jimbo lote, huku vyama vingine vikiwa havina kabisa madiwani.
Nchemba anasema wingi huo wa madiwani, ni mtaji tosha wa kuivusha katika uchaguzi huo ikiwa wana-CCM hao watatumika vizuri, kwa kuwa kila walipo kuna wanachama, mashabiki na wapenzi wa CCM nyuma yao.
Lakini pia Nchemba anasema, hata ikitazamwa idadi ya wajumbe walioshiriki katika vikao vya mchakato wa kuwachagua wagombea jimboni, wa CCM walikuwa zaidi ya mara tatu ya wajumbe wa CHADEMA.
Hali hiyo anasema inadhihirisha kwamba CCM itakuwa na kura nyingi zaidi ya CHADEMA baada ya uchaguzi, ukiachilia vyama vingine ambavyo anasema vinachechemea, na vingi vimeibuka kwa ajili ya uchaguzi tu.
Jambo jingine ambalo linampa moyo ya ushindi Nchemba, ni kura za maoni zilizotumika kumpata mgombea wa CCM, ambazo hazikuacha makovu ya uhasama baina ya wagombea kama ambavyo imekuwa ikijitokeza katika michakato mingine.
Anasema baada ya kura za maoni, wajumbe wote waliokuwemo katika kinyang'anyiro cha kuwania kuteuliwa na Chama kuwa mgombea wa ubunge wa jimbo la Igunga, wote wameridhika na kumuunga mkono Dk. Kafumu, ambaye ameteuliwa kuwa mgombea wa CCM.
"Tangu Dk. Kafumu apite, wote walioingia katika kura za maoni wameendelea kumuunga mkono katika kila hatua, na wameahidi kuwa naye bega kwa bega katika kampeni.
Mratibu huyo wa kampeni za CCm katika jimbo hilo, anasema hiyo inamaanisha kuwa hakuna mpasuko uliojitokeza", alisema Mwigulu.
Anasema kutokana na kuzibwa mwanya huo wa mpasuko katika Chama baada ya kura za maoni, sasa vyama vya upinzani kama CHADEMA havitaweza kupata tena kura za chuki kutoka kwa wana-CCM, ambazo wamekuwa wakizipata katika uchaguzi mwingine.
Mbali na Dk. Kafumu, baadhi ya wana-CCM walioshiriki kinyang'anyiro cha ndani ya Chama na kuwemo katika kura za maoni ni Jaffar Omari, Shamsu Abraham, Hamis Mapinda na Ngassa Nicholaus, ambao baada ya uteuzi wa Dk. Kafumu kufanywa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, wametamka kumuunga mkono.
Nchemba anasema pia CCM imefanikiwa kuzima fitima zilizokuwa zimeanza kupandikizwa na CHADEMA kwa wananchi, ili ionekane kama serikali ya CCM inakandamiza wananchi katika zao la ufuta na mazao mengine ya biashara, zimefanyiwa kazi.
Rostam
Katika mtazamo kwamba huenda aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo aliyejiuzulu, Rostam Aziz, akawa msaada kwa wapinzani kujipatia kura za ubwete, haumo mashiko baada ya mbunge huyo wa zamani kuonekana kuendelea kukiunga mkono Chama chake Cha Mapinduzi kwa namna mbalimbali, pamoja na kwamba si za wazi kwa sasa.
Bila shaka Rostam hawezi kuwa mwepesi kuchukua uamuzi wa kusaidia vyama vya upinzani kama CHADEMA, hasa akikumbuka kwamba ni viongozi wa CHADEMA ndio walikuwa wa kwanza kumnyooshea kidole kwa bidii zote tena katika mikutano ya hadhara nchi nzima wakimshutumu kwa ufisadi.
Pengine ni kwa kutambua wabaya wake halisi, ndio sababu hata baada ya kutangaza kujivua ubunge na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Rostam alitangaza kinaga ubaga kwamba ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa CCM.
Kauli hiyo inathibitisha kwamba hawezi kukisaliti Chama chake, hali inayothibitisha kwa CCM itaendelea kuteza katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Oktoba 2 mwaka huu.