Monday, November 14, 2011

Habari za Kitaifa

Waliochakachua’ mtihani kidato cha nne kizimbani
Imeandikwa na Shangwe Thani, Shinyanga; Tarehe: 24th October 2011 @ 00:32 Imesomwa na watu: 452; Jumla ya maoni: 1

WATU wanne wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga, kwa tuhuma za kufanya udanganyifu katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka huu kwenye shule ya Sekondari ya Paji iliyopo wilayani Meatu.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Meatu, Mwendesha Mashitaka Rajabu Botea alidai kuwa washitakiwa kwa pamoja katika sekondari ya Paji wilayani Meatu walikula njama za kufanya udanganyifu kwenye mtihani wa taifa wa kidato cha nne kinyume cha sheria.

Waliopandishwa kizimbani ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya sekondari ya Nganza iliyopo mkoani Mwanza, Eunice Edward (19), Mkuu wa Shule ya sekondari ya Paji, Pius Mabula (32), msimamizi wa chumba cha mtihani katika shule ya sekondari ya Paji ambaye pia ni mwalimu wa sekondari ya Bukundi, Zakaria Mashauri (26).

Mwingine ni mama wa nyumbani aliyemaliza elimu ya sekondari mwaka 2004 ambaye kwa sasa ameolewa wilayani Meatu, Mbuke Masanja (24), aliyejisajili kwenye shule ya sekondari hiyo kwa lengo la kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka huu kwa kutumia jina la mwanafunzi aliyefukuzwa shule hiyo kwa sababu ya kupata ujauzito, Kulwa Igunzile.

Inadaiwa kuwa Eunice alikwenda wilayani Meatu mkoani hapa akitokea mkoa wa Mwanza kwa lengo la kumsaidia kumfanyia mtihani wa taifa wa kidato cha nne, Mbuke kwenye sekondari ya Paji kinyume cha sheria na kanuni na taratibu za mitihani.

Inadaiwa kuwa katika mtihani huo, Eunice alifanikiwa kufanya mitihani sita kati ya tisa aliyotarajiwa kuifanya mpaka alipokamatwa na kamati ya usimamizi wa mitihani ya wilaya ya Meatu ilipofika kwenye chumba cha mtihani shuleni hapo na kumkuta Eunice akiendelea kufanya mtihani huo.

Washitakiwa wote wanne wamekana mashitaka hayo na kuachiwa kwa dhamana mpaka Oktoba 26 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.

No comments:

Post a Comment