Sunday, November 13, 2011

siasa au SIHASA 1

Pinda- Chadema badilikeni, acheni maandamano
Imeandikwa na Na Waandishi Wetu, Arusha na Dodoma; Tarehe: 10th November 2011 @ 19:58 Imesomwa na watu: 717; Jumla ya maoni: 1




WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amekitaka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiache uanaharakati na maandamano ya mara kwa mara kama kinataka nchi isonge mbele.

Pinda alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kutoka kwa wabunge katika mkutano wa tano wa bunge unaoendelea, Dodoma, akisema Chadema inahitaji kuteremka chini na kuangalia maslahi ya nchi kwa mapana zaidi.

Alielezea kukerwa na mtindo inaoutumia wa kufanya maandamano kila kukicha na kaulimbiu yao ya ‘Peoples power (Nguvu ya umma)’ kwamba hazioneshi dhamira ya kweli ya kuleta amani.

Alisema ipo haja kwa Chadema kubadilika, ili kuipa imani Serikali kukiona kuwa ni chama makini na kinachohitaji kumaliza mgogoro uliopo.

Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) aliyesema kuwa mgogoro wa vyama vya CCM na Chadema wa umeya wa Arusha umevuka mipaka na kusambaa nchi nzima na kuwa wa kitaifa.

“Hivi sasa (mgogoro huo) umevuka mipaka ya kivyama na umekuwa wa kitaifa na kusambaa maeneo mbalimbali ya nchi na kwa kuwa (Pinda) ulilitambua hilo na ukaandika barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na baada ya kupokea majibu ya CCM je, upo tayari kutoa maelekezo mengine ama ushauri mwingine ili upande wa pili ujue hatima ya suala hili na ijue hatua za kuchukua?” Alihoji Mnyika.

Pinda alijibu; “Ndugu Mnyika usilikuze jambo hili kama limesambaa nchi nzima, si kweli, lakini kikubwa ninachokiona katika mazingira ninayoyaona, wenzangu wa Chadema mnayoyafanya kinachohitajika ni dhamira ya kweli kwa pande zote mbili, kwa namna mambo yenu mnavyoyafanya huoni dhamira ya kweli.

“Kila siku maandamano kila mahali sisi tulioko serikalini tunapata tabu sana, tunataka kufanya kazi nyingine ambazo zinahitajika, lakini muda wote unakaa unafikiria maandamano.

“Mteremke chini kidogo, tuanze kuona maslahi mapana ya nchi, tuone ni mambo gani ya msingi yanahitajika, kwa pamoja twende mbele,” alisema.

Alisema tabia ya uanaharakati ya Chadema inanipa taabu sana, lakini kama umakini utakuwapo, haoni tatizo watu kukaa na kuzungumza suala hilo, “katika hali ninayoiona mimi ‘peoples power’ kila kukicha si nzuri, haiwezekani.”

Kuhusu mgogoro wa umeya wa Arusha, Pinda alisema kama Chadema inaona haja ya kukaa kwa mazungumzo iandike na kuelezea maeneo inayoyaona yanahitaji kujadiliwa.

Awali Pinda alieleza kuwa aliingilia mgogoro huo kwa kumwelekeza Msajili akutane na vyama hivyo, kuona maeneo ya kuzungumza akiamini tatizo litapatiwa ufumbuzi lakini CCM ilijibu kwa barua kwamba haioni cha kuzungumza.

Akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), aliyetaka kufahamu kwa nini Serikali imemzuia Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kutoka rumande na kuathiri utalii, alisema Mbunge huyo hakuzuiwa bali mwenyewe alikataa dhamana.

Alisema wanatarajia Novemba 14 kesi hiyo itakapotajwa, Mbunge huyo anaweza kuachiwa na kuongeza kuwa utalii haujaathirika kutokana na vurugu hizo, lakini akawataka wananchi kuzingatia amani ili utalii huo usiathirike.



Chadema, Polisi kumaliza mgogoro Arusha
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 10th November 2011 @ 19:59 Imesomwa na watu: 554; Jumla ya maoni: 2




CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Jeshi la Polisi mkoani Arusha, wamekubaliana kukaa na kutafuta mwafaka wa kinachodaiwa kuwa mgogoro katika mkoa huo.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema hayo jana nje ya Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Arumeru, alipokuwa akielezea mazungumzo yake juzi na viongozi waandamizi wa Polisi.

Alisema polisi wamekubali kukaa meza moja na Chadema kuzungumzia mgogoro wa Arusha na kwa sababu wamekubali kuzungumza nao, wanasubiri mazungumzo hayo yafanyike.

"Tunachosema kwa sababu wametuomba tukae meza moja na tuyamalize haya mambo, basi nasi tumesitisha maandamano ya nchi nzima na mikutano.

Maandamano hayo yaliyokuwa yameitishwa nchi nzima kufanyika jana, yalisitishwa na Jeshi la Polisi kwa kuwa hayakuwa yametolewa taarifa lakini pia yalilenga kuvunja amani.

Akizungumzia kikao hicho, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema kikao hicho wanakisubiri kwa hamu na endapo hakutakuwa na utekelezaji wa maazimio yatakayofikiwa, chama hicho kitaamua la kufanya.

Dk. Slaa alisema, kwa sababu Polisi imewaomba, busara lazima zitumike kwa muda kwani vikao walivyofanya ni vingi na hakuna mwafaka uliofikiwa.

Bila kueleza kama ikishindikana wataondoa busara au la, Dk. Slaa alisema wanasubiri kuona maazimio ya kikao hicho, ambacho hakijaitishwa, yakitekelezwa na kwa kiasi gani.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, alithibitisha kufikiwa kwa uamuzi huo katika kikao chao cha juzi na Mbowe

Wakati hata kikao chenyewe hakijaitishwa, Mbowe alitanguliza vitisho kuwa endapo hakuna utekelezaji wa yatakayoamuliwa basi wataendelea na maandamano yao kama kawaida.

“Jana (juzi) waliniomba nifanye kazi ya kusitisha maandamano na mikutano nami nikafanya hivyo na tunasubiri utekelezaji wa maazimio tutakayoafikiana na kama hakuna utekelezaji basi wataendelea kutupiga mabomu, kubambika kesi na sisi tutaendelea kudai haki," alisema Mbowe.

Akizungumza akiwa nje ya Mahakama baada ya kupata dhamana, Mbowe alisema jana alizungumza na polisi kwa saa kadhaa juu ya mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa mgogoro wa umeya Arusha.

Jana Mbowe alifikishwa katika Mahakama hiyo akikabiliwa na mashitaka mawili ya kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya Polisi.

Akisomewa mashitaka hayo na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Haruni Mategane, ilidaiwa kuwa alifanya mkusanyiko usio halali saa 11 alfajiri Novemba 7 na 8 katika viwanja vya NMC akiwa na washitakiwa wenzake ambao walishafikishwa mahakamani ambao ni Dk. Slaa, Tundu Lissu na wafuasi wao 28.

Katika mashitaka ya pili alidaiwa kukaidi amri ya Polisi ya kutakiwa kutawanyika eneo la uwanja wa NMC, lakini baada ya kusomewa mashitaka hayo mawili, Mbowe alikana.

Wakili anayewatetea, Method Kimomogolo, alimwomba Hakimu Devotha Kamuzora kutoa masharti kama waliyopewa awali Dk. Slaa, Lissu na wenzao 28 ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na ahadi ya dhamana ya Sh milioni 5.

Hakimu Kamuzora alisema masharti ya dhamana ya akina Dk. Slaa yako wazi na hatimaye Mbowe alidhaminiwa na kesi kupangwa kutajwa Novemba 22.

Juzi Mbowe alijisalimisha Polisi kutokana na Jeshi hilo kumtaka afanye hivyo, baada ya kudaiwa kuwakimbia wakati akina Lisu wakikamatwa mbaroni.

Mbali na mgogogro huo pia Mbowe alidai walizungumzia suala la maandamano yaliyotangazwa juzi na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Kuhusu maandamano hayo, Mbowe alisema , polisi walimhoji kama alitoa kauli za kuitisha maandamano na mikutano ya Chadema nchi nzima lakini akasema hakutoa kauli hiyo bali zilitolewa na viongozi wengine wa Chadema.

Mazungumzo hayo aliyodai kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa Polisi, pia yalizungumzia kusitisha maandamano yaliyotangazwa awali na Chadema nchi nzima.


Chadema njia mnayofuata Arusha siyo
Imeandikwa na Yona Maro; Tarehe: 10th November 2011 @ 15:59 Imesomwa na watu: 76; Jumla ya maoni: 3



MIMI ni kati ya watu wanaofuatilia sana habari na taarifa mbalimbali za mkoa wa Arusha hasa Arusha Mjini ambako nina maslahi nako, si mimi tu.

Hata wengi wenye maslahi na Arusha Mjini hasa wawekezaji, watakuwa na hofu kama ile
niliyokuwanayo mimi, ya amani na utulivu kuendelea mjini hapo, ili biashara zao na shughuli zao zingine ziweze kutendeka kama kawaida.

Kwa kweli tangu Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), aingie madarakani, amefanya machache ambayo kwa sura ya vijana, wanaweza kuona ni sahihi, kwa mfano kutumia ubunge wake kuruhusu Wamachinga kuuza bidhaa mitaani.

Hajatenga eneo maalumu kwa ajili ya Wamachinga hao au kuwa na mpango na suala hilo hata kwenye hotuba tu, hivi sasa Arusha ni mji unaoanza kuwa mchafu; kabla yake mji ulikuwa unang’aa.

Sasa hivi jina la Arusha kama Geneva ya Afrika ndilo hilo linakimbia, yale mauaji ya watu watatu katika maandamano ya Chadema Januari, mgomo wa daladala wa juzi na huu mkesha wa viwanja vya NMC ni taa tosha kutuonesha jinsi baadhi ya viongozi wanavyotaka kutumia
mabavu kwa kisingizio cha nguvu ya umma kutimiza matakwa yao kisiasa.

Kwanza Lema mwenyewe ndiye alitaka kwenda rumande huku akijua kitendo hicho ni hatarishi, huku viongozi wa Chadema nao wakijua ni kosa, leo wanalazimisha Mahakama
imtoe Lema huku wakijua suala hilo liko kwenye vyombo vya sheria na ni lazima sheria ichukuwe mkondo wake!

Kitendo hiki kitaumiza wengine endapo litatokea jambo lolote kutokana na mkusanyiko mkubwa wa watu, au hata makundi mengine ya kihalifu, yanaweza kutumia fursa hiyo kutekeleza hujuma zao dhidi ya nchi zetu hasa kundi la al Shabaab ambalo ni hatari katika eneo hili la Afrika Mashariki.

Nawaomba viongozi wa Chadema hasa wale wa Arusha Mjini kuangalia mienendo yao kwa
maslahi ya jimbo la Arusha Mjini, mkoa wa Arusha na Tanzania kwa jumla, huyo mbunge hakuchaguliwa kwa ajili ya kulumbana na vyombo vya Dola, amechaguliwa kwa ajili ya
kuwakilisha wananchi wake bungeni kwa njia zilizonyooka ambazo yeye mwenyewe aliapa akiwa bungeni.

Viongozi wa Chadema waangalie alama za nyakati, muda unaweza kupita na jimbo la Arusha likakosa maendeleo na hatimaye kukimbiwa na watu na Chadema mnaweza kupoteza jimbo hilo kwa aibu mwaka 2015.

Heshimuni mamlaka iliyoko madarakani pamoja na vyombo vya Dola kwa maana hata nyie mtakuja kushika Dola, sasa hivi ndio muda mzuri wa kuoneshana adabu na heshima na kuleta kuaminiana kati ya vyama na vyombo vya Dola.

Arusha ina wadau wengi ambao wanahitaji utulivu ili kuendesha shughuli zao wakiwamo wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ambao wanaathirika na vurugu za kila mara ambazo si tu zinahatarisha maisha yao lakini hata mali zao wanazowekeza.

Hivi ni nani kwa mwaka mzima atakalia ghasia, maandamano, mauaji na majeraha, asifanye kitu kingine cha uzalishaji mali? Inapotokea vurugu mjini ni wazi maduka yanafungwa, ofisi zinafungwa na huduma mbalimbali zinasimama, hiyo yote ni kwa faida au hasara?

Wanasiasa kama wa Chadema wasidhani kuwa kuita umati wa watu na kuwachochea vurugu na
kisha kukamatwa, ndiko kujifungulia mlango wa kuingia madarakani, la hasha, zipo njia nyingi za kudai haki, si lazima fujo na kukaidi amri halali za Dola.

*Mwandishi wa Wazo hili amejitambulisha kama msomaji wetu na mwanajukwaa la mtandao wa kompyuta.





Jumla Maoni (3)

Maoni Nakuunga mkono mwandishi wa makala hii arusha sasa imegeuka kuwa ukanda wa gaza na walio sababisha hilo ni CHADEMA mimi si mkazi wa Arusha lakini najua kuwa Arusha ni lango la kuingilia watalii lakini chadema mnasababisha mlango huo uanze kujifunga taratibu ni milango ya nchi jirani ianze kufunguka kwa kasi mwe na uchungu na nchi yenu sio uchungu wa kuchukuwa madaraka kwa kutumia neno "nguvu za uma" jamani okoeni Arusha.Acheni malumbano jengeni Arusha

Maoni Chadema hiki siyo kipindi cha kudai Uhuru,ni kipindi cha watu kushughulika na uzalishaji na hatimaye maendeleo ya nchi yetu. Waache hizo tumechoka nao sasa.

Maoni Kaka hongera sana kwa ufafanuzi mzuri sana Kusema ukweli hawa chadema me nawaona kama wababa ishaji kwani kama hajui kusoma hata picha hawazioni Enyi wafuasi wa chadema Mna macho lakini hamuoni mnamasikio lakini hamsikii hata kidogo

No comments:

Post a Comment